Unaiendeshaje biashara yako?

Sep 18, 2015


Leo nitajadili kuhusu udhibiti wa mali (stock control). Yafaa kukumbuka kuwa, ukinunua  mali kwa ajili ya biashara yako unahitaji kuidhibiti ili iweze kutoa matokeo mazuri ya kibiashara.
 
Udhibiti wa mali (stock control) maana yake ni utaratibu katika biashara unaohusisha upokeaji mali, uwekaji kumbukumbu wa mali, uhifadhi wa mali, upangaji wa mali, uhakiki wa mali na uagizaji wa mali.
 
Makala iliyopita  ilizungumzia moja ya tatizo kubwa linalowakabili  ni kuhusu kutokutunza kumbukumbu za biashara, walikumbushwa kuwa mali bila daftari hupotea bila habari, huwezi kukumbuka kil akitu juu ya shughuli zako za kila mara.
 
Udhibiti wa mali ni muhimu katika biashara, kwani husaidia kufahamu ni wakati gani, vipi na kwa nini unahakikisha huishiwi mali ili usiwakere wateja wako. Pia itakusaidia kupunguza hasara inayoweza kusababishwa na wizi, uharibifu au uchakavu.
 
Udhibiti wa mali, husaidia biashara kuainisha aina za bidhaa na vitu ambavyo wateja wanahitaji. Kwa kuangalia mwenendo wa mtiririko wa mali, unaweza kutofautisha kati ya bidhaa zinazotoka haraka na zile zinazotoka taratibu.
 
Mali katika biashara inadhibitiwa kwa kuweka kumbukumbu sahihi. Kwa mfano kuweka kadi za mali, orodha ya mali, ankara na kumbukumbu za mauzo taslimu za kila siku katika biashara yako.Usifanye biashara kwa mazoea kwa kujaza tu duka lako. 
 
Ili kuwa na udhibiti wa mali wenye kujenga ufanisi, kuna njia mbalimbali wajasiriamali wanakumbushwa kuzizingatia ili kujenga ufanisi katika biashara zao. Njia hizi ambazo hutoa mwongozo wa kudhibiti mali zipo tano, nazo ni kama zifuatavyo:
 
Weka kiasi sahihi cha mali
Kumbuka kuweka kiasi sahihi cha mali. Mjasiriamali unakumbushwa kuweka kiasi sahihi cha mali, usiweke mali nyingi mno au mali chache. Mali nyingi zinazuia fedha zako zisizunguuke na mali chache zinaweza kwisha na ukasimama katika mauzo.
 
Tunaposema usiweke mali nyingi au chache maana yake, mjasiriamali anapaswa kuzingatia mahitaji ya wateja wake.Mara zote yapasa kufahamu mwenendo wa hitaji la soko lako.Pia mjasiriamali anapaswa kuwa makini katika uagizaji mali.
 
Bidhaa ipi inatoka haraka
Jiulize bidhaa zipi zina mzunguko mzuri? Mjasiriamali unashauriwa kuelewa utokaji wa bidhaa katika biashara yako.Wajasiriamali wanakumbushwa kuweka bidhaa zinazotoka haraka na hii itafanya mauzo kuwa mazuri, hivyo kuingiza fedha nyingi katika biashara.
 
Kwa kuwa kuna mali zinazotoka taratibu lakini zikiwa zinatoa faida nzuri, yafaa kuweka kiasi kidogo cha mali zinazotoka taratibu ili kukwepa kukwamisha fedha zako katika mali. Vile vile kumbuka kutoa bei zenye punguzo ili kuvutia wateja na kumaliza haraka. 
 
Unapanga vipi bidhaa zako?
Jiulize namna  unavyopanga bidhaa zako au unapanga tu? Kumbuka upangaji mzuri wa bidhaa zako ni namna nzuri ya kuwavutia wateja. Mjasiriamali kupanga bidhaa  katika hali ya unadhifu itasaidia wateja kuona kwa urahisi pia kurahisisha kuhesabu na kuhakiki.
 
 
Tunapozungumzia upangaji wa bidhaa kama njia ya kudhibiti mali, yafaa ieleweke kwamba, kwa bidhaa au vitu vinavyofanana yafaa vionyeshwe au kuwekwa kwa ukaribu, na inapasa kuepuka kuweka mali hasa vitu vinavyoharibika kwa muda mrefu.
 
Fanya ukaguzi wa mali.
Jijengee utaratibu wa kukagua mali katika biashara yako. Ni muhimu kukagua mali mara kwa mara ili kufahamu kama biashara yako ina bidhaa zinazohitajika na hakuna mali inayokosekana, pia itakusaidia kugundua kama kuna tatizo lolote katika bidhaa.

 
Weka kumbukumbu za mali
Kumbuka kuweka kumbukumbu za mali. Mjasiriamali yakupasa kuacha kufanya biashara kwa mazoea, jitahidi kuweka kumbukumbu za mali. Hii ni changamoto kubwa inayowakuta wajasiriamali wengi katika biashara, yafaa kuiangalia kwa kirefu zaidi.
 
Kumbukumbu za mali ni maandishi yanayoeleza kilichotokea kwa mali katika biashara. Inamaanisha  kumbukumbu ya mali inayoingia na inayotoka katika biashara. Kama unahitaji kufanikiwa ni vizuri kujua mwenendo mzima wa mali katika biashara.
 
Yafaa ieleweke kuwa, wajasiriamali wanaweza kuweka kumbukumbu za mali katika nyaraka na namna mbalimbali. Kwa ajili ya kuwakumbusha wajasiriamali, leo tutaangali namna mbili ambazo zimekuwa zikitumika  kuweka kumbukumbu za mali. Njia hizo ni kadi ya mali na orodha ya kuhesabu mali.
 
Kadi ya mali hutumika kuweka taarifa juu mali. Inahusisha mambo mengi kama vile, jina la mali, bei kununulia, bei ya kuuzia, kiasi kipya cha kuagiza, tarehe ya mauzo, mali iliyotoka na salio.
Share on :
 
Copyright © 2015 Raizoni Blog
Distributed By My Blogger Themes | Design By SPARTO Inc Team