
IDADI ya wagonjwa wa kipindupindu imezidi kuongezeka katika jiji la Dar es Salaam, ambapo wamefikia 405 kwa wilaya mbili za jiji hilo. Katika Manispaa ya Kinondoni kuna jumla ya wagonjwa 348 tangu kuanza kwa ugonjwa huo, hali iliyosababisha manispaa hiyo kupiga marufuku uuzwaji wa vyakula holela ikiwa ni jitihada za kupambana na ugonjwa huo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Afya wa manispaa hiyo, Mathias Kapizo alisema, idadi hiyo imekuwa ikiongezeka ambapo jana walipokea wagonjwa 35 kutoka katika kaya tofauti zilizopo ndani ya manispaa hiyo.
“Mpaka sasa idadi ya wagonjwa ni 348 kwa wilaya ya Kinondoni peke yake. Kutokana na ongezeko la ugonjwa huu tumepiga marufuku uuzaji wa vyakula holela mchana ili kupambana na nzi wanaosababisha maambukizi na badala yake biashara hizo zifanyike usiku,” alisema.
Alisema marufuku hiyo ni mpaka pale hali itakapotulia na ugonjwa huo kuisha. Wagonjwa waliopelekwa katika kambi ya wagonjwa hao iliyopo Mburahati, hakuna aliyepoteza maisha kwa kuwa waliweza kufika kwa wakati kabla hali zao hazijawa mbaya na kupewa huduma ya kwanza na matibabu mengine.
Manispaa hiyo ilipata wagonjwa 65 wa kipindupindu na walifanya jitihada za kujitoa katika ugonjwa huo kwa kutoa huduma za hali ya juu kwa wagonjwa hao. Kata za manispaa hiyo ambazo zimekumbwa na ugonjwa huo ni pamoja na Buguruni, Tabata Shule, Ilala na Kisiwani. Taarifa kutoka wilaya ya Temeke hazikupatikana jana.