Freddy Macha
Mwanadamu anahitaji malezi, mavazi na chakula.
Hana haja ya kuondoka kwao kama vitu hivyo vya msingi vipo. Viongozi wa Ulaya sasa hivi wanakinzana wakishangaa namna wakimbizi na wahamiaji wanaoyakwepa maeneo yenye tafrani Afrika na Mashariki ya Kati, hususan, Syria... Mwanadamu ahitaji malezi, chakula na mavazi kuishi, ila haya huendana na utamaduni.
Hivi karibuni nilikuwa safari ndefu ya kikazi sehemu mbalimbali huku huku Uzunguni.
Kwa kuwa nilihitajika kubeba zana mbalimbali za kikazi ilibidi kuendesha gari badala ya kutegemea usafiri wa kadamnasi yaani matreni na mabasi. Kawaida usafiri huo huwa mzuri nchi zilizoendelea. Magari moshi ni ya kasi na safi kabisa.
Unapoendesha gari utakupambana na balaa la misongamano, ajali na uchovu. Ingawa barabara za Ulaya kubwa na safi, kiasi cha magari barabarani huwa cha kutisha, hasa ajali zinapojiri. Ingawa ajali za uzembe hazipo sana nchi zilizoendelea, zikitokea huwa mbaya sana.
Sababu gani?
Barabara kubwa zinazoitwa “highway” (Marekani), “auto route”(Ufaransa), “autobahn” (Ujerumani), “estrada” (Hispania na Ureno), “motor way” (Uingereza) si za mchezo. Kwa kuwa ni pana zenye migawanyiko ya wastani wa nne kwa mpigo hukupa uchaguzi. Ukienda kasi sana unatumia upande mmoja, ukitaka kupita magari mengine unatumia mstari wa pili na unaofuatia huwa wa kujitayarisha ama kutoka barabarani kwenda njia nyingine au kupisha yanayokwenda haraka. Mstari wa mwisho ni wa mabasi na malori ya mizigo au magari yanayokwenda polepole.
Utaratibu huu ni mzuri tofauti na nchi zetu zinazoendelea, magari hayagombanii nafasi au mstari mmoja wa njia.
Sasa tatizo, hukoleza ajali zinapotokea.
Mwendo ni wa kasi. Gari moja likigonga jingine yanayofuata huingia palepale na mara kwa mara hutokea zaidi ya mashine ishirini kuvaana kwa mpigo.
Faida ya kwenda na usafiri wako hukupa nafasi au uhuru wa kutembelea utakapo ukimaliza kazi. Wakati huu niliamua kuwasalimu marafiki na ndugu wakiwamo Watanzania wakazi huku.
Unapoingia majumbani mwa watu ndiyo unapotambua tofauti za kitamaduni.
Tuanze na wenzetu wasio Waafrika.
Umefika salama. Ukafunguliwa mlango...
Pale ambapo Mwafrika mwenzako atakupokea mzigo mlangoni, wenzetu hawana tabia hiyo. Labda utaulizwa, “Nikusaidie kubeba?” Lakini si mazoea kuparamia mzigo wa mgeni na kuuingiza ndani. Hata akija kwako hakutugemei umpokee mzigo kumsaidia. Labda awe mzee au mgonjwa. Atataka aubebe mwenyewe. Huu ni utamaduni wa kila mtu na lwake. Utamaduni uliotokana na hali ya hewa ya baridi ; kila kiumbe hujaribu kujisetiri asitetemeke au kugeuka barafu. Saikolojia ya mali binafsi na ubepari.
Umo.
Umeshaingia ndani sasa.
Ukakaa.
Kawaida jambo la kwanza humpa mgeni pole.
Sijawahi kulisikia neno hili ndani ya msamiati wa lugha kadhaa za kigeni nlizojifunza. Tafsiri yake haipo. Labda ipo nchi nyingine za Kiafrika. Ila hisia ya kupewa ahueni, uafadhali na furaha unayoipata kupitia “pole”.
Labda wenzetu weupe hupeana mabusu na kukumbatiana zaidi yetu. Wengine hadi wanaume hugusana mashavu, mathalan Waarabu na Warusi. Mgeni utaulizwa habari za safari. Kwetu utatayarishiwa maji ya kuoga. Hayo pia wenzetu wanayo. Utaoneshwa bafu liko wapi.
Ila mbali na kukosa “pole” usishangae ukaulizwa : “Je, mipango yako nini?” Swali hili huwa kali sana kama hujalizoea. Lina maana je, utalala? Je, utakula? Je, utakaa hapa siku ngapi? Wenzetu wanao utamaduni wa kuangalia siku za mbele. Kwa Mmatumbi swali kama hilo hutoa nishai. Hatuna desturi za kuwatoa nishai wageni. Humuulizi mgeni je, atakula? Chakula kipo kimsingi, bila maneno mengi.
Mila ya kupanga ya mbeleni imetokana vilevile na mabadiliko ya hali ya hewa. Wenzetu Ulaya na Marekani wana majira manne tofauti kila mwaka. Jua hafifu na mvua za manyunyu (sasa, Oktoba, yaani “Autumn”), baridi kali (kipupwe chenye barafu, “Winter”) , baridi wastani na maua kuchanua (“Spring”) na hatimaye kiangazi (“Summer”). Wamezoea kujipanga. Desturi hii huendana na mfumo wa kibepari na kibiashara. Ndiyo sababu Wazungu hufuata utaratibu na ratiba. Sisi tuna majira mawili makuu. Jua na mvua. Zaidi ya hayo, hutegemea labda nyanda za juu, au mabadiliko ya ghafla ya mazingira.
Mgeni.
Umeshaulizwa hali, ukatulizwa pengine na kikombe cha chai.
Kama nyumba ya wenyeji ina watoto, yule mdogo kabisa ataamriwa akuoneshe vyumba vyote. Sisi hatuna desturi ya kumwonesha mgeni vyumbani. Wenzetu hutaka kukujulisha mazingira yakoje, kusudi ikitokea dharura kama moto ujue pa kutokea. Huenda wakati ukitambulishwa nyumba kukawepo na mnyama kama mbwa au paka. Mtoto atataka hata umpapase na kumgusa na kumpa salamu na mapenzi. Kuna wakati niliwahi kukaribishwa na wenyeji waliofuga fuko na tumbili, sebuleni.
Utakoma kama hujazoea wanyama kama sisi Afrika tunavyowaweka wanyama nje kulinda makazi. Wenzetu hulala nao! Mnyama huhesabiwa sehemu ya familia. Iko siku nilikaa mahali sahani ya paka pia ilisafishwa sehemu moja na vyombo vyetu. Ilinitoa nishai. Lakini mgeni utafanyaje? Tofauti za kitamaduni hizo.
Umefika wakati wa kula.
Yaweza kuwa mawili.
Usishangae ukaulizwa utakula nini. Na kama ulishawahi kuja hapo, huenda ukaambiwa uingie tu jikoni ukajitengenezee chakula. Kwetu huduma hiyo muhimu hufanywa na wanawake hatimaye kutuletea msosi. Wanawake wa huku mara nyingi huwa na mtazamo wa “hakuna kazi za wanawake na wanaume.”
Wenzetu wamezoea kupeana uchaguzi.
Tuchukue zawadi mathalan.
Zawadi yoyote huchangamkiwa.
Kwa wenzetu desturi ya zawadi ni kinyume. Sherehe za harusi, kuzaliwa, Pasaka au Krismasi, watoto au maharusi, huorodhesha zawadi wanazozitaka. Uchaguzi huu unatokana na jamii kuwa na shibe. Kwa nini umletee mtu zawadi ambayo huenda akawa nayo? Wazungu wanapenda kutoa zawadi zenye manufaa. Kushtuliwa kwa zawadi ambayo uliitaka lakini hukuitegemea. Ni kazi kwako mtoaji kufanya utafiti kwa kuulizia ulizia rafiki au ndugu za utakayemzawadia. Nini fulani anapenda au kuhitaji? Na unapoileta sasa huwa umecheza karata mfalme.
Mmmh.
Ukarimu ni ukarimu.
Viwango vya makaribisho huwa vilevile duniani. Moyo. Lakini viwango hivi, mwananchi, huegemea mila na desturi. Tukumbushane. Siku zote zingatia, penda, ijue, ithamini mila, desturi na utamaduni wako.
London, 30 Septemba, 2015
-Bpepe: gmacha52@gmail.com
-Tovuti: www.freddymacha.com