Serikali ya Nepal imetoa wito wa kuwepo hali ya utulivu nchini humo
baada ya tetemeko kubwa la ardhi kuikumba tena nchi hiyo na nchi jirani
hapo jana. Maafisa wa jeshi la majini la Marekani wamesema helikopta ya
Marekani ya kutoa misaada iliyokuwa na abiria wanane haijulikani iliko
baada ya tetetemeko hilo jipya. Tetemeko hilo la kiwango cha 7.3 katika
kipimo cha Ritcher limeongeza masaibu ya raia wa Nepal wiki chache tu
baada ya jingine kuwaua maelfu ya watu. Maafisa wa Nepal wamesema kiasi
ya watu 48 wameuawa hapo jana na kiasi ya wengine 1,176 wamejeruhiwa
huku majengo kadhaa yakiporomoka. Wafanyakazi wa shughuli za uokozi
wametumwa katika maeneo yaliyoathirika na mkasa. India na China pia
zimeripoti kuathirika na tetemeko hilo la ardhi.
Idhaa ya DW