![]() |
| Mwandishi Freddy Macha |
Sehemu ya magharibi ya London siyo sawa na ya Afrika Mashariki. Majira yanapobadilika na mwangaza wa jua kutumbukia; huja na mbwembwe zake. Tuko msimu wa baridi kali yenye barafu ukanda wa kaskazini wa dunia. Kiza huanza kukonyeza saa tisa alasiri. Hiyo saa kumi na moja jioni tunayosimuliana giza finyu lilishapiga deki. Mchana, kwaheri.
Lakini shughuli za wanadamu zilezile. Maduka hayajafungwa. Duka tunalotazama ni la hawa wamachinga pembe ya barabara kuu. Wahindi wenye maduka wanajuana kwa vilemba. Mmachinga wetu ni Mpakistani. Ana kameza kake kadogo mbele ya upenu wa mita tano kwa mapana ya mita moja, kajaza simu za mkononi, vibiriti, sigara. Jambo la ziada ni simu na vipengele vyake. Betri, waya, mikebe ya kuzifungia; kila unachokililia kwa simu yako; ongeza yeye fundi.
Iko siku aliniambia kwao alihitimu ualimu ila
sababu ya rabsha za kisiasa akatupilia mbali taaluma yake akafuata ndugu
aliowajua London. Ukimchunguza hajafikisha miaka ishirini na tano.
Yuko hapa miaka miwili. Alianza kaduka bila meza na mifuko ya plastiki.
Akiuza kadi za Lyca Mobile, kampuni ya bei rahisi inayotumiwa sana na
wageni Uzunguni. Mtanzania anapopiga simu kutoka huku mara nyingi
anatumia mtandao wa Lyca. Simu za viganjani ni biashara nzuri. Tuseme
suala zima la kompyuta na mitandao ni kitengo chenye masilahi.
Watazameni vijana wawili waliounda WhatsApp. Mmoja
kwao ni Ukraine. Walianza kitu kidogo tu lakini leo mabilionea baada
ya kumuuzia Myahudi anayemiliki Facebook uvumbuzi wao. Vijana wa
Kitanzania mnaosoma kuweni wabunifu. Jaribuni kutafiti na kujua nini
kinatakiwa. Uchunguzi wa kina badala ya domo sana na siasa za
malalamiko.
Basi, Mpakistani alichangamkia umachinga na hizo
kadi. Baada ya miaka miwili, hauzi tu vidato vya simu. Anazikarabati.
Ukimuuliza kajuaje, atakwambia alipofika Uingereza alikwenda chuo
akasomea ufundi miezi kumi. “Mengine ni utundu tu...” Kaduka hakiishi
wateja. Hula hapo hapo, kutwa, kasimama akichora fedha.
Siku hii tunayohadithiana nilitaka asafishe
mfereji wa simu yangu uliokuwa na mushkeli. Wakati nimetoa pochi
n’namlipa paundi tano alizotaka (kama shilingi elfu kumi na mbili);
kando yangu kajipachika bonge la mtu. Mwamba. Niliisikia sauti yake
nzito kabla ya kushuhudia tambo lake. Macho yanakodolea zile fedha
ninazomlipa Mpakistani.
“Nipe paundi moja nikanunue maji. Nitakurudishia.”
Kamngurumia Mmachinga. Sauti nzito. Ilinikumbusha
mchezaji fulani wa sinema. Nilipogeuka nikamaizi nimemfikia begani.
Mweusi sana. Hajavaa nguo chafu. Yuko kawaida. Kiingereza chake kina
lafudhi hakika ya Kiafrika. Mpakistani kamwambia hana hiyo paundi moja
ambayo ni kama ya shilingi elfu mbili na kitu za Tanzania.
“Nipe bwana nitakurudishia!” Jamaa kazoza, na kusonya juu.
Hapo sasa ananizonga na miye maana kanafasi
tulichosimama wawili hakitutoshi. Kawaida huku Uzunguni mteja anapokuwa
akihudumiwa, wale wanaomfuata husubiri zamu yao katika foleni. Hivyo
jamaa hajafuata utaratibu. Ongeza kiburi.
Mpakistani kapokea fedha niliyompa. Akaiweka
kibindoni. Upesi akachakura makabrasha nyuma ya bidhaa zake, akarejea
na chupa ndogo ya maji. Akampa jamaa. Bure.
“Haya chukua, maji. Hela sina, samahani.”
Ombaomba si kapewa maji aliyotaka? Sasa...
Sasa...kwani atayapokea kwa shukrani?
“Hayo siyo maji niliyohitaji. Nataka yenye gesi. Koo langu haliko sawa. Nipe yenye gesi bwana!”
“Sina yenye gesi. Samahani!” Bado mwenye duka anampa jamaa chupa ya maji.
Mwafrika mwenzangu si kaja juu?
Akasonya. “Nakuomba basi unipe paundi moja. Paundi
moja tu. Nikatafute maji. Koo langu kavu. Nina mafua. Hii baridi
inanimaliza. Nitakurudishia!” Mimi sasa narejeshewa simu yangu.
Najitayarisha kuondoka.
Mpakistani kafura.
“Samahani sana!...” ....Kaanza.
Tukumbushane mila na desturi. Neno samahani,
yaani “sorry,” kwa Waingereza ni muhimu sana. Utamaduni na kauli yao
wenyeji hawa waliotutawala zamani, inakusihi ulijue, ulimanye,
ulithamini. Samahani yaani Sore, ni neno doooogo unapashwa kulikariri,
kulikumbuka, kulitaja, kuliheshimu. Ukikanyagwa. Ukikanyaga. Ukipigwa
kikumbo. Ukigonga kikumbo. Ukiomba, ukiombwa, ukikataa, ukikubali;
ukikosea, ukikosewa. Kwa Mwingereza hufunga mashtaka na kuondoa kisirani
na kutoelewana. Ni kama sisi kumpa mwenzio pole. Amefiwa, amekukosea,
umemkosea; kaugua, umeugua. Na kadhalika.
“Samahani, “ akaanza Mmachinga. “Hili hapa ni
duka. Siwezi kuwa nagawa hela kwa kila mtu. Biashara hii. Si kanisa au
msikiti. Nimekupa maji hutaki. Nifanyeje?”
Mwafrika (maana nilikadiria lafudhi yake nzito ni
Mmatumbi mwenzangu) pandikizi la mtu, akapiga kite, akapandisha mabega,
akasonya mara ya tatu, akafutua mdomo; akatoa kidole cha shahada
alichomnyooshea, kikunguru, kijana wa Kipakistani.
“Yaani nakuomba paundi moja tu unanikatalia? Nipe
bwana nitakurudishia! Nyinyi watu sijui kwanini mna roho mbaya namna
hii? Wabinafsi...”
Niliwahi kuandika kuwa wenye maduka huwa
hawapotezi muda kujibishana. Huyu kakaa kimya. Alikuwapo mteja mwingine
anatusubiri nyuma ya mstari.
“Naweza kukusaidia? ....”
Mteja akahudumiwa. Akalipa. Akayeyuka.
Wakati akiondoka, yule Mmatumbi mwenzangu, kero
inamtafuna, utadhani utitiri wa kuku, sasa anatingisha kichwa akitukana
kikwao. Matusi. Misonyo. Huyoooo...hamsini.
Mmachinga akanigeukia.
“Unaona? Sisi tunafanya kazi usiku na mchana wengine wanakuja kututukana?”
Naam. Hawa Wahindi na Wapakistani wanachukiwa
sana na baadhi ya watu weusi. Ukweli nafasi za biashara zipo kila
mahali. Bora ujue utaratibu. Jamii ya kibepari hii. Ukitaka cha
mvunguni, chutama. Walihamia walipofukuzwa Uganda na marehemu Idi Amin
mwaka 1971 na 1972. Wengine mathalan huyu Mmachinga, wamefuata ndugu zao
waliohamia miaka 50 au 60 iliyopita toka bara Asia. Wapo waliokuja
kusoma wakazamia. Nidhamu. Alfajiri hadi magharibi. Iwe Jumapili sikukuu
ya Idd El Fitr, Krismasi, mapumziko ya kiserikali. Wamo kazini.
Hawajui kudorora. Weka sasa ushirikiano baina yao. Hujengana. Sisi?
Kusengenyana. Kulogana. Kutaka vya bure.
Wiki iliyopita tulizungumzia yanayoendelea
Nigeria. Bajeti ya ulinzi wa kitaifa, ni kali kuzidi majeshi mengi
barani. Lakini “wameshindwa” (kama kweli ni kushindwa) kupambana na
waasi wanaoteketeza makazi na kuua wanawake, watoto wa shule na
maskini. Hapo hapo viongozi wanaomba msaada kwa Wazungu. Neno gani ndugu
msomaji tutumie kuiita hulka, mwenendo, msimamo na tabia hii ya baadhi
ya wanasiasa wetu Afrika?
