“Nimeamua kuuza figo ili nipate pesa za kufanya
biashara. Figo yangu naiuza kwa Sh50 milioni tu, bei yangu ni poa
kabisa, siyo kama huyu jamaa”.
“Nataka nikipata pesa nioe, umri nao umekwenda.
Nashindwa kuoa kwa sababu sina pesa za kumtunza mwanamke,” anasema
Bangili ambaye ana elimu ya kidato cha nne.
Si ajabu kusikia mtu amejiua kwa sababu tu ya ugumu wa maisha. Wengi wanafikia uamuzi huo baada ya kuhisi hawana msaada mwingine wa kupunguza makali ya maisha. Hata hivyo, kujiua siyo njia sahihi ya kupambana na changamoto.
Si ajabu kusikia mtu amejiua kwa sababu tu ya ugumu wa maisha. Wengi wanafikia uamuzi huo baada ya kuhisi hawana msaada mwingine wa kupunguza makali ya maisha. Hata hivyo, kujiua siyo njia sahihi ya kupambana na changamoto.
Hali imekuwa tofauti kwa kijana Armstrong Bangili
aliyeahirisha uamuzi wake wa kutaka kujinyonga na sasa anafikiria kuuza
figo yake. Anasema anaishi maisha ya tabu tangu alipofukuzwa kazi katika
benki moja mwaka 1998.
Kabla ya kutekeleza ‘jaribio la kujiua’ wiki
iliyopita, Bangili alisoma Gazeti la Mwananchi, toleo la Januari 3.
Alipokutana na habari ya Andrew Chimulimuli kutoka Morogoro aliyetangaza
kuuza figo yake kwa Sh90 milioni.
Anasema alipata tumaini kuwa hata yeye anaweza
kuuza figo yake na kuondokana na umaskini unaomkabili kwa sasa. Hata
hivyo, anakiri kuwa hana elimu yoyote juu ya athari za kutoa figo au
jinsi ya kuishi baada ya kutoa figo.
“Nimeamua kuuza figo ili nipate pesa za kufanya
biashara. Figo yangu naiuza kwa Sh50 milioni tu, bei yangu ni poa
kabisa, siyo kama huyu jamaa,” anasema Bangili huku akionyesha makala ya
Chimulimuli ambayo ilimbadili mawazo.
Bangili mwenye umri wa miaka 45 anasema amekuwa
akiishi kwa kuombaomba miaka yote, jambo linalowakera watu na yeye pia.
Anaeleza kuwa amejaribu kutafuta kazi maeneo mbalimbali lakini amekosa.
Anabainisha kuwa akipata fedha hizo ataanzisha
mradi wa kilimo cha mbogamboga na ufugaji wa nyuki. Anaamini kuwa ana
uwezo wa kuendesha shughuli hiyo na kujiongezea kipato zaidi ndani ya
muda mfupi.
“Yaani nikipata hiyo hela nitanunua shamba la
ekari tano huko Bagamoyo au Tegeta, nitaanzisha kilimo cha mbogamboga na
kufuga nyuki. Baada ya miaka mitatu mbona nitakuwa bilionea!” anasema
huku akicheka.
Kijana huyo anayeishi Sinza, Dar es Salaam
anaonekana kudhoofu mwili akisema hiyo inatokana na kula mlo mmoja na
wakati mwingine kutokula kabisa. Anasema mbali na kuwa ndugu zake hawana
uwezo, pia wamemchoka kwa sababu wamemsaidia kwa muda mrefu.
Bangili anatoka kwenye familia ya watoto wanne,
akiwa ndiye mkubwa. Anasema wadogo zake wengine wana maisha yao na
wanajimudu kwa kipato kidogo wanachokipata.
Mara nyingi amekuwa akipokea msaada kutoka kwa
waumini wa Kanisa la Waadventisti wa Sabato, lakini anasema sasa
amechoka kuombaomba, anahitaji kuwa na kazi ya kumuingizia kipato.
“Nataka nikipata pesa nioe, umri nao umekwenda.
Nashindwa kuoa kwa sababu sina pesa za kumtunza mwanamke,” anasema
Bangili ambaye ana elimu ya kidato cha nne.
“Nimekata tamaa kabisa ya kuishi, nyumba ninayoishi nililipiwa
kodi na rafiki yangu niliyesoma naye Shule ya Sekondari Kinondoni
Muslim. Wazazi wangu walifariki muda mrefu, nilitaka kuuza nyumba ili
nipate mtaji, shangazi akanikataza.”
Mkurugenzi wa Taaasisi ya Figo nchini, Jaji
Frederick Werema aliwahi kukaririwa na gazeti hili akishangaa kuona
baadhi ya watu wakiuza figo zao, jambo ambalo alisema ni kinyume cha
sheria.
“Kuuza figo ni kosa la jinai, lakini siyo hivyo
tu, kutoa figo lazima ufuate taratbu za kisheria na za kitabibu,”
alisema Jaji Werema miezi kadhaa iliyopita.
Athari za kutoa figo
Taasisi ya Utafiti wa Figo ya Uingereza
inabainisha kuwa mtu anayeishi na figo moja anaweza kuishi kama wengine
endapo atalinda mwili wake dhidi ya nguvu ya msukumo wa damu.
Inashauriwa mtu huyo asishiriki kwenye michezo kama vile mpira, mieleka,
ndondi au mchezo wa kuteleza kwenye barafu ili kujiepusha na hatari ya
kudhurika.
Taasisi hiyo inaeleza katika jarida lake la
mtandaoni kuwa watu wengine huzaliwa wakiwa na figo moja na wengine
hutoa ili kuwasaidia wapendwa wao ambao figo zao zote hazifanyi kazi.
Jarida hilo linafafanua kuwa baadhi ya watu
wanapata matatizo baada ya kutoa figo zao ikiwa ni pamoja na shinikizo
la damu. Hata hivyo, athari hizo zinaelezwa kujitokeza muda mrefu
baadaye.
Jarida hilo linasisitiza uangalizi wa karibu kwa
watoto waliotolewa figo moja likisema athari wanazoweza kupata ni
kuongezeka kwa protini nyingi kwenye mkojo, pia figo zao kushindwa
kufanya kazi wanapofikia umri wa utu uzima.
Jarida jingine la kuchangisha figo ili kuokoa
maisha ya watu wenye matatizo (Give a Kidney) la Uingereza, linabainisha
hatua kadhaa za kufuata kabla figo haijatolewa na mtindo wa maisha ya
kuishi baada ya kuondolewa kwa figo moja.
Linaeleza kuwa kabla ya kutolewa figo, mhusika
anachukuliwa vipimo vingi ikiwamo afya ya mwili na akili. Vipimo hivyo
hulenga kuchunguza kama mtoa figo yupo kwenye hali nzuri kiafya kwa kuwa
na uzito unaohitajika, pia kutokuwa katika msongo wa mawazo. Mtoa figo
anapewa msaada ya kisaikolojia ili aishi vyema baada ya kutoa figo.
Jarida hilo linaeleza kuwa wengi wanaotoa figo huathirika kisaikolojia
kwa hofu ya kifo.
Vipimo vingine ni mkojo pamoja na damu. Vipimo
hivyo huchunguza kama mtoa figo ana maambukizi mengine ya magonjwa,
kiwango cha protini kwenye mkojo na kundi la damu la mtoa figo.
Kadhalika, mtoa figo anapigwa picha ya X-Ray
kuchunguzwa kama mapafu na moyo wake viko katika hali nzuri. Pia,
anachunguzwa kama figo zake zote ziko sawa. Baadhi ya watu huzaliwa
wakiwa na figo moja, pengine bila wao wenyewe kujua.
Jarida hilo linabainisha kuwa mtu mwenye figo moja au mbili ambazo hazifanyi kazi vizuri, hana sifa ya kuchangia figo. Pamoja na vipimo vingine, mtu anaruhusiwa kutoa figo yake baada ya daktari kujiridhisha kuwa atakuwa salama.
Jarida hilo linabainisha kuwa mtu mwenye figo moja au mbili ambazo hazifanyi kazi vizuri, hana sifa ya kuchangia figo. Pamoja na vipimo vingine, mtu anaruhusiwa kutoa figo yake baada ya daktari kujiridhisha kuwa atakuwa salama.