Mfumo thabiti wa Uwajibikaji ni moja ya
jawabu muhimu sana katika kuhakikisha Taifa linaondokana na ufisadi na masuala
mengine yanayorudisha nyuma maendeleo ya Tanzania. Kazi za mwisho za Kamati ya
PAC katika Bunge la Kumi zilisheheni mambo mengi muhimu katika mchakato
endelevu wa ujenzi wa mfumo thabiti wa uwajibikaji nchini kwetu.
Taarifa ya Mwaka iliyojadiliwa na
kupitishwa na Bunge wiki iliyopita ndio ilikuwa taarifa yetu ya mwisho katika
Bunge hili. Kama kawaida mwaka 2015 ulianza kwa ziara za kukagua miradi na
hatimaye kukutana na maafisa masuuli wa Wizara na Mashirika ya Umma ili kukagua
mahesabu yao na kufuatilia utekelezaji wa maagizo ya wakaguzi na Kamati.
Kipindi hiki ni muhimu sana kwangu
kwani kwa vyovyote vile ni kazi yangu ya mwisho kufanya kama Mwenyekiti wa PAC,
nafasi niliyoichukua mwezi Machi mwaka 2013. Kabla ya hapo nilikuwa Mwenyekiti
wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) kuanzia Februari mwaka 2008
mpaka Februari mwaka 2013. Katika Maisha yangu ya miaka 10 Bungeni, nimetumikia
uongozi wa kamati hizi kwa miaka Saba na Nusu. Hata hivyo leo natafakari kazi
ya wiki nne tu na nilichojifunza katika siku hizo.
Wiki ya Kwanza, tulitembelea miradi ya
njia za Reli na Mashamba ya Miwa ili kuongeza uzalishaji wa Sukari nchini.
Tulikwenda mkoani Morogoro katika Wilaya za Kilosa na Kilombero. Tulijulishwa
kuhusu mahitaji ya fedha nyingi katika ujenzi wa Reli ya Kati ambapo ili
kukarabati mtandao Reli iliyopo zinahitajika jumla ya shilingi 500 bilioni kwa
miaka mitatu mfululizo ($800m). Vilevile zinahitajika dola za Kimarekani $6
bilioni kujenga reli mpya ya kisasa (standard gauge). Wiki mbili baada ya
kumaliza ziara hiyo, niliona picha ya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta akikagua
ujenzi wa Reli ya kisasa nchini humo. Nilipoangalia picha yangu na wajumbe
wenzangu katika kijireli chetu, nilicheka kicheko cha huzuni sana. Nimejifunza
kwamba nchi yetu inaweza kusonga mbele iwapo tu tutaamua kujinyima baadhi ya
maeneo ili kuendelea kwenye maeneo mengine. Fedha inayopotea katika kutoa
misamaha ya kodi (tshs 1.9 trilioni ) peke yake, kwa mwaka mmoja inamaliza ukarabati
wa Reli yote ( Kigoma – Tabora – Dar es Salaam na Tabora – Mwanza ).
Wiki hiyo pia tulitembelea kiwanda cha
Sukari cha Kilombero na kukutana na Wakulima wa Miwa. Tanzania ina nakisi ya
Sukari ya takribani tani 120,000 – 200,000 kwa mwaka.
Uzalishaji wa ndani wa tani 300,000
hautoshelezi mahitaji ya wananchi na hivyo twalazimika kuagiza Sukari kutoka
nje ya nchi ambayo husamehewa kodi. Kwa mwaka Tanzania husamehe kodi ya zaidi
ya shilingi 200 bilioni katika Sukari peke yake. Fedha hii ingeweza kujenga viwanda
kadhaa vya Sukari na hivyo kuachana kabisa na uagizaji na badala yake kuuza
nje. Nimejifunza mengi sana katika kushughulikia suala la Sukari nchini.
Nimeona namna ambavyo mfumo mzima wa Serikali ulivyo na ganzi katika kupata
suluhisho la kudumu.
Hivi sasa Serikali inataka uagizaji wa Sukari ufanywe na
wazalishaji wa Sukari, majawabu ya namna hii ni majawabu ya kugawana pato
nyemelezi (rent seeking). Jawabu la kudumu la sekta ya Sukari ni kuongeza
uzalishaji wa ndani kwa kufungua viwanda vipya maeneo yenye miwa ya ziada hivi
sasa, kutoa ruzuku kwa viwanda ili kupunguza gharama za uzalishaji na hatimaye
kuwa na bei nafuu kwa walaji na kufungua mashamba mapya ili kuzalisha ziada na
kuuza nje kwa ajili ya kupata fedha za kigeni.
Tulijadili kwa kina sana changamoto
zinazoikabili sekta ndogo ya kilimo cha Korosho.
Ukaguzi Maalumu ulionyesha
kuwa kuna unyonyaji mkubwa wa wakulima ikiwemo kupewa pembejeo zilizoisha muda
na kutofikishiwa pembejeo kabisa. Pia upotevu mkubwa sana wa Korosho na suala
zima la kuuza korosho ghafi nje ya nchi. Utafiti uliofanywa na African Cashew
Alliance unaonyesha kuwa Tanzania hupoteza zaidi ya dola za kimarekani 110
milioni kila mwaka kwa kuuza korosho ambazo hazijabanguliwa.
Ikumbukwe kuwa Tanzania ilikuwa na
viwanda 12 vya kubangua Korosho na vyote viliuzwa katika zoezi la ubinafsishaji
na sasa vimekuwa ni maghala ya kuhifadhia Korosho. Tulielekeza kuwa mapato
yanayotokana na tozo ya mauzo ya Korosho nje (export levy) yatumike kujenga
viwanda vipya vya korosho kwa kutumia teknolojia mpya kutoka Vietnam ambapo
viwanda vidogo vidogo vitajengwa kuanzia vijijini na kuzalisha ajira nyingi na
kuondoa umasikini. Nimejifunza kwamba Korosho peke yake inaweza kuingiza fedha
za kigeni katika nchi yetu kwa thamani ya zaidi ya dola za kimarekani 500
milioni kwa mwaka. Mwaka 2014 Tanzania imezalisha tani 200,000 za Korosho,
rekodi ambayo haijawahi kufikiwa tangu tupate Uhuru.
Korosho inaweza kuondoa
umasikini kwa watu wa mikoa ya Kusini iwapo Viongozi wakiamua iwe hivyo.
Ilituchukua siku 2 kujadiliana na
Mamlaka ya Mapato Tanzania kuhusu mahesabu yao ya mwaka wa fedha ulioishia
Juni, 2013. Sababu kubwa ilikuwa ni mjadala kuhusu misamaha ya Kodi. Kama
nilivyoeleza hapo juu, tulijulishwa kuhusu misamaha mingi ya kodi kuendelea
kutolewa mpaka kufikia jumla ya shilingi 1.9 trilioni katika mwaka wa fedha
ulioishia Juni, 2014. Kamati pia ilijadili Taarifa ya ukaguzi maalumu kuhusu
misamaha ya kodi na kugundua kuwa misamaha mingi inatumika ndivyo sivyo.
Nimejifunza kuwa tukiendelea kusisitiza uwazi na uwajibikaji tunaweza kupunguza
tatizo hili la misamaha holela ya kodi. Tuliagiza kuwa kuanzia sasa, katika
kila
Taarifa ya makusanyo ya TRA kila mwezi, pia taarifa ya misamaha ya mwezi
huo itolewe kwa umma. Hii itasaidia kuonyesha ni mapato kiasi gani yangeweza
kukusanywa bila ya misamaha na kama misamaha hiyo ni muhimu na inatumika
ipasavyo.
Mifano hii michache ya Reli, Sukari,
Korosho na Misamaha ya Kodi imenikumbusha changamoto nyingi ambazo nchi yetu
inazo na namna bora ya kukabiliana na Changamoto hizo. Mfumo thabiti wa
Uwajibikaji ni suluhisho endelevu dhidi ya changamoto hizi. Kamati ya PAC
imeshiriki kikamilifu kujenga mfumo huo. Kazi bado kubwa lakini inaendelea.
Zitto Zuberi Kabwe
Source: https://zittokabwe.wordpress.com/