Makala: Freddy Macha

Feb 27, 2015

Utoto na ujana ni  muhimu sana katika maisha ya mnyama, mdudu na mwanadamu. Ndiyo sababu kila mila na desturi duniani huunda misemo kuhimiza nyakati hizi. Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Samaki mkunje,  angali mbichi. Asiyesikia la mamaye hufunzwa na walimwengu.  Siku njema huonekana asubuhi...nk.

Misemo inanirejesha nyuma nilipoanza kidato cha kwanza,  sekondari Ilboru, mwaka 1969. Ilboru ilishika mpini  wa skuli bora kuzidi zote Tanzania. Si ajabu baadhi ya viongozi wetu, Mhe George Mkuchika na Frederick Sumaye walisoma hapa. Angalia. Nilipomaliza darasa la saba, Kaloleni, Arusha, tulichaguliwa wawili kuendelea sekondari. Mwenzangu Profesa Faustin Maganga, alikwenda kwingine mimi nikachopea, Ilboru.

Hiki ni kipigo kikubwa sana kwa ambao hawakuchaguliwa. Takwimu za 1968 zilikuwa asilimia 13 tu za waliovuka daraja hilo la uzi. Mbali na alama za juu sana, kimasomo, ilibidi uwe na bahati. Wengine 87 kati ya mia waliishia majumbani. Leo takwimu zimesepa zaidi. Shirika la Elimu ya Sayansi na Utamaduni la  Umoja wa Mataifa (UNESCO) linatueleza asilimia 43 ya watoto Afrika hawako shule.  

Takriban nusu ya watoto wa Kimatumbi hawasomi. Si ajabu tumejaza vibaka na madereva  wanaolewa na kuvuta bangi na kusababisha ajali mbaya sana. Bila elimu tosha, mambo magumu, Afrika.


Inatia moyo, hata hivyo, kusikia wasichana wa Kitanzania, walifanya vizuri kidato cha nne mwaka jana.

Siku za mwanzo mwanzo Ilboru tuliitwa Mugya, neno  tuliloambiwa ni la Kiganda lililoimanisha mgeni.  Leo kila nikiwauliza  Waganda tafsiri ya Mugya hujikuna kichwa. 
Sina hakika kama lilibuniwa tu na kaka zetu waliotutangulia au la. Ilikuwa neno la kashif, sanifu na uonevu wa kisaikolojia. Liliudhi; lakini mgeni ni mgeni tu. Maonevu ya kisaikolojia ni sehemu ya utoto na ujana. Yakubidi ugangamale. Ndani ya matani haya mabwenini au darasani niliwasikia wanafunzi  wawili, Mugya wenzangu, wakicheka cheka kila saa. 


Ingawa tambo zao zilitofautiana, kitabia walipenda masihara. Mmoja alikuwa rangi ya chungwa; Mmeru; mwenzake mtu wa pwani, mweusi, Mbondei wa  Tanga. Wote warefu, wembamba.  Miaka hamsini iliyopita tofauti  baina ya watu wa bara na wa pwani, ilikuwa  mkasa.   Ila hawa wawili waliufuta ukinzani huo kwa utani utani.  Mmeru alisema Kiswahili  chenye lafudhi ya mikoani, milimani Arusha; Mbondei aliburuza Kiswahili fasaha cha Mwambao. .  Tofauti za kidini na kimikoa, hali kadhalika, hazikuathiri urafiki, ulimbwende na ucheshi wao. Tulikuwa darasa moja; tukaendelea  hadi , 1972.


Nikahamia Mzumbe, Morogoro; wao wakasonga kidato cha tano, Mirambo, Tabora. Kama tulivyosema awali, jua kheri la mtoto huchomoza asubuhi... 

Ilboru ilikuwa ...mmh... labda nianze kwa kutongoa sentensi niliyoisoma ukumbi wa “Jamii Forums” mwaka 2008 kuhusu elimu ya zamani....”Siku hizo,shule zilikuwa shule,walimu wakiwa walimu,hakuna cha tuition wakati huo wala wizi wa mitihani.”


Ilboru iliajiri waalimu wa kila pembe ya dunia. Tulifundishwa vizuri.

Mwalimu mkuu,  marehemu  Dk Anza Lema,  alisisitiza usafi, kusoma sana (“kuchimba”) na nidhamu.  Dk Lema alikuwa Mwafrika wa kwanza Ilboru iliyosifika kama shule ya Kizungu na Kikristo.  Alikuwepo mwalimu Victoria Chitepo wa Zimbabwe aliyetufundisha fasihi ya Kiingereza. Baada ya Uhuru (1980) akateuliwa Waziri wa Elimu, Zimbabwe. 

Mama Chitepo alitusukuma  kupenda vitabu. Tulipoingia kidato cha tatu, mwalimu mkuu mpya Geoffrey Mushi (mwaka jana alifiwa na mkewe aliyekuwa mwalimu pia) alimpokea marehemu Lema.  Mwalimu Mushi alihimiza ukakamavu.  Mchakamchaka asubuhi, uzalendo na utaifa. Kutokana na mstari huo  na kifua mbele  tulimkatia jina la “Chest.”


Mwaka 1971 Tanzania ilipotimiza miaka kumi ya Uhuru, mambo yalikuwa moto nchini. Kati ya heka heka ni mashindano ya uandishi bora na wanafunzi wawili darasa letu wakawika kijogoo. Insha ilitwaaliwa na Vince Shaidi; Ushairi ukanyakwa na Rashid Othman. Ni huyu Rashid Othman (leo Mheshimiwa  Othman)  mcheshi mcheshi wa Tanga, rafiki yake Mmeru, mrefu, Albert Kanuya. Rashid Othman na Vincent Shaidi walikwenda Ikulu, Dar es Salaam wakapewa tuzo na Mwalimu Nyerere. 

Lilikuwa tukio kubwa kwa bwana wadogo, kwenda Ikulu kupewa mkono na Rais Nyerere. Ni muhimu kuzingatia namna mwalimu mkuu,  Geoffrey “Chest” Mushi alivyowaonea fahari wanafunzi wake. Ilijenga ari ya kusoma, kushinda  na kuipenda nchi.

Mwaka huo huo, sasa Rashid Othman aliandika mchezo wa kuigiza ulioangalia maisha ya Mwafrika aliyekwenda kusoma Uzunguni akarudi na nyodo na majivuno. Akabadili jina lake la kuzaliwa, Jiwe Risasi kuwa “Stone Bullet.” Kisa kiliiva na sisi wengine tukajiunga kufanya maigizo. ..

Tamthiliya ilipendwa sana Ilboru kutokana na ujumbe mzuri uliooana na matakwa ya Mwalimu Mkuu Mushi na maadili ya kizalendo. Tuliuonyesha shule jirani. Baadaye Rashid Othman aliandika nyimbo mbalimbali zilizorekodiwa na bendi maarufu ya Tanga, Atomiki Jazz. Mojawapo ni “Joyce” uliopigwa sana Redio Tanzania.


Wakati haya yakiendelea tulikuwa na kundi lililoitwa “The Gringos” pale Ilboru. Tulichanganya kila kabila. Mwangaza wa mkoa wa Ziwa Magharibi, Mmbulu, Chotara wa Kigiriki na Kiluguru, Mpare, Mbondei na miye Mchagga. Chungu hiki cha makabila kilionesha namna tulivyovuka mstari na kuupenda “Utanzania” zaidi.


Ni mengi ya kuhadithia, lakini, muhimu  ni namna malezi ya mtoto na kijana hujenga mustakabali wake. Wakati Bwana Othman akifanya kazi Ubalozi wa Tanzania, London, (miaka thelathini baada ya Ilboru),  tulikaa na kukumbushana shule. Je nani alikuwa hai, nani anafanya nini, yupi kafariki? Mbali ya tuzo ya mashairi aliyozawadiwa na Mwalimu Nyerere 1971, ilikuwa maajaliwa, kumwona miaka hii na hadhi tofauti.


Mwalimu Nyerere  alipofariki hapa London 1999, Rashid Othman sasa mmoja wa maofisa rasmi wa serikali alisimama na wenzake Ubalozini kando ya jeneza la mwasisi wa taifa. Mwaka 2004 mwanae alipofunga ndoa,  nilimtazama Mama Rashidi, nyanya mtu, akitabasamu. 

Fahari ya mwanae, jicho kwa mjukuu. Ni mama huyu, Bi Othman  aliyefariki karibuni akiwa na umri wa miaka 83.Mama aliyemlea mtoto na kumshuhudia akiwa Mkurugenzi wa Usalama nchini. Mazishi yalihudhuriwa na viongozi kadhaa akiwamo Rais Jakaya Kikwete.
Share on :
 
Copyright © 2015 Raizoni Blog
Distributed By My Blogger Themes | Design By SPARTO Inc Team