Vijana wanaofunga ndoa nchini wapungua

Feb 13, 2015

Dar es Salaam. Ugumu wa maisha unaozikabili familia nyingi nchini unaelezwa kusababisha athari nyingi kwa maendeleo ya jamii. Athari hizo zimegawanyika katika makundi mbalimbali yakitofautiana na mitazamo na hali ya maisha.

Hata hivyo baadhi ya athari hizo zinawakumba vijana ambao ndiyo kundi kubwa la Watanzania moja ikiwa kupata hofu ya kuamua kutekeleza au kuamua mambo mbalimbali ikiwamo kufunga ndoa.

Tatizo hilo ni ukweli unaowekwa hadharani na maelezo mbalimbali ikiwamo takwimu za kitaalamu za Sensa za Idadi ya Watu na Makazi iliyofanyika nchini mwaka 2012, iliyobainisha kuwa asilimia ya watu waliooa au kuolewa imepungua.

Taarifa za msingi za kidemografia, kijamii na kiuchumi ya matokeo muhimu yaliyojitokeza kwenye Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 zinaonyesha kwamba asilimia ya watu waliooa au kuolewa imepungua.


Takwimu za Sensa

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali (OCGS),Zanzibar hali hiyo inaweza kuwa imesababishwa na ugumu wa maisha na ugonjwa wa Ukimwi.

“Asilimia ya watu waliooa au kuolewa imepungua kutoka asilimia 54 mwaka 2002 hadi asilimia 51 mwaka 2012. Hii inaweza kuwa imesababishwa na ugumu wa maisha na athari za ugonjwa wa Ukimwi,” imeeleza taarifa hiyo.

Inaeleza kuwa asilimia 58 ya watu wenye umri wa miaka 15 na zaidi nchini wameoa  au kuolewa au kuishi pamoja na wenzi wao.

Matokeo hayo muhimu yanabainisha kwamba  idadi ya watu walioachana au kutengana imepungua kutoka asilimia tano mwaka 2002 mpaka asilimia nne mwaka 2012, hali ambayo ilielezwa kuwa ni ishara ya kudumu kwa ndoa kadiri miaka inavyoongezeka.            
Share on :
 
Copyright © 2015 Raizoni Blog
Distributed By My Blogger Themes | Design By SPARTO Inc Team