| SMS Königsberg ikiwa katika pwani ya Dar es Salaam |
SMS Königsberg ilikuwa ni meli kubwa ya kivita ya Wajerumani katika koloni lao la Afrika Mashariki.
Ilitengenezwa na Jeshi la Wanamaji la Ujerumani na
kukamilishwa mwaka 1906. Aprili 1914 meli hii ilipangiwa majukumu ndani
ya Afrika Mashariki na ilisafiri kutoka Ujerumani hadi bandari ya Dar
es Salaam ambako pia ilipangwa kuwa ni sehemu ya maadhimisho ya sherehe
za kukamilika kwa ujenzi wa reli ya kati kutoka Dar es Salaam hadi
Kigoma mwaka 1914.
Ilikuwa ni meli kubwa yenye uwezo wa kukimbia
kilometa 44.6 kwa saa ambao ulikuwa ni mwendo mkubwa sana kwa wakati
huo. Ilikuwa na bunduki kubwa kumi na mabomba matatu makubwa ya kutolea
moshi ndipo wenyeji walipoiita Manowari ya Bomba Tatu wakiitofautisha na
meli nyingi za wakati huo zilizokuwa na mabomba mawili ya kutolea
moshi.
Simulizi zinasema kuwa mara tu Konigsberg ilipotia
nanga bandarini Dar es Salaam mji mzima ulizizima. Mamia ya watu
walifurika pale Magogoni na sehemu za Kigamboni kuishangaa meli hiyo
kubwa ya aina yake kwa wakati huo.
Hali ilikuwa hivyo kila ilipokwenda iwe Tanga,
Bagamoyo, Lindi au Mtwara. Manowari ya Bomba Tatu ilikuwa ni kivutio cha
aina yake. Kweli ilikuwa ni gumzo kila kona na alama ya nguvu za
Wajerumani katika Afrika Mashariki.
Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia ilipozuka Julai 1914,
Konigsberg ilijaribu kuharibu misafara ya biashara ya Uingereza na
Ufaransa katika bahari ya Hindi.
Chini ya Unahodha wa Maxi Loof, mnamo tarehe 20
Septemba 1914, Konigsberg iliishambulia na kuizamisha meli ya kivita ya
Uingereza HMS Pegasus katika mapambano ya Zanzibar.
Upungufu wa makaa ya mawe uliathiri ufanisi wa
meli hii na kuifanya iweze kuzamisha meli moja tu ya kibiashara kwenye
kampeni nzima ya Afrika Mashariki ambayo ni HMS City of Winchester.
Nahodha wa Königsberg aliamua kuificha meli yake
kwenye delta ya mto Rufiji ili kuzifanyia matengenezo injini zake lakini
kabla ya matengenezo kukamilika meli mbili za uchunguzi za Kiingereza
ziitwazo Mersey na Severn ziliigundua Königsberg pale kwenye delta na
kuiharibu kwa kuipiga kwa makombora.
Mnamo tarehe 11 Julai 1915, meli zile za Uingereza
zilisogea karibu kabisa na kuiharibu vibaya Königsberg, hivyo nahodha
wake Loof na askari waliosalia wakaamua kuiharibu Königsberg ili
isiangukie mikononi mwa Waingereza.
Askari waliosalimika katika mapambano yale ya
Rufiji Delta walichukua bunduki zake zote 10 na wakaungana na Kamanda
wao wa vikosi vya ardhini Paul von Lettow-Vorbeck katika vita vya
msituni vilivyodumu hadi mwisho wa Vita va Kwanza ya Dunia.
Kati ya mwaka 1963 hadi 1965 timu ya wataalamu
waliibomoa Königsberg kwa ajili ya chuma chakavu na mabaki yake
yakazamishwa chini ya mto Rufiji. Huo ukawa mwisho wa meli hii iliyoteka
hisia za wengi Afrika Mashariki, hususan Tanzania ya wakati huo.
Mwandishi: Rajab Kipango
Mwandishi: Rajab Kipango