Mwandishi Freddy Macha akitumbuiza
wakati wa tamasha la Carnival London, Agosti, 2012.
Picha na Urban Pulse Creative
Media
Miaka arobaini au
hamsini iliyopita nakumbuka waliopenda mahusiano na wageni walikuwa zaidi
wanaume. Wanawake waliojamiiana na wageni waliitwa malaya, na wachache ni wale
tu waliofanya kazi mahoteli makubwa ya kitalii kutafuta ajira.Mathalan
nakumbuka miaka ya
Sitini naSabini, Tanzania ilijazana wakimbizi. Sera ya TANU na siasa ya Azimio
la Arusha ilisaidia walioathirika na udhalimu wa kikoloni, ubaguzi nk. Toka
Kongo, Afrika Kusini,Palestina, Malawi, Marekani, Uganda, nk.
Wengi wa wakimbizi
wa Kongo (iliyoitwa Zaire enzi za utawala dhalimu wa Jemadari Joseph Mobutu)
walikuwa wanaume, hasa wanamuziki, waliohusudiwa sana na wanawake wetu.
Mzaire aliongea Kiswahili -chenye lafudhi ya Kifaransa na
Kilingala- kilichomfanya avutie kwa utofauti na mwanaume wa Kitanzania.
Au wakimbizi wa Afrika Kusini, Namibia na Zimbabwe. Tuliwaita Waafrika
Kusini, “Wasoweto” kutokana na harakati au machafuko ya kitongoji cha
Soweto mjini Johannesburg mwaka 1976. Wasoweto walikuwa tofauti. Walivalia
suruali pana pana. Waliongea Kiingereza fasaha. Vijana wa kiume na kike tuliona
akheri kubwa kwenda na Wasoweto kuliko wazalendo wenzetu. Miye kwa mfano
nilikuwa na sahiba aliyependa fasihi, mashairi na kupiga muziki.

Awali nilipata
shida sana – na miaka yangu ishirini na moja au miwili-, kupata sahiba wa kike
aliyependa fasihi na muziki. Wasichana wa rika langu walitaka kwenda baa, kunywa
bia – na vile ka- mshahara kangu ka uanahabari magazeti ya Chama (Uhuru na
Mzalendo) kalivyokuwa nyau, haikuwa rahisi kubembelezana na dada zangu, hata
wawe wazuri namna gani. Aghalabu, kadri uzuri ulivyozidi ndivyo karaha
ilivyoongezeka.
Wasoweto hawakujali.
Azma yao ilidai uhuru; walipenda utamaduni wa michezo na kusoma vitabu. Mkikosa
fedha ya basi au teksi mnatembea tu kwa miguu mkiongelea haiba ya mawingu, maua
waridi, misufi, twiga, muziki wa Jazz, Taarabu, hadithi za Ali Nacha na siasa
za Wapalestina. Mkifika hivyo hivyo ugali kwa maharage na ndizi kisukari.
Mnasoma mashairi ya Shaaban Robert na Christopher Okigbo (Mshairi wa Nigeria
aliyefariki angali kijana mwaka 1967) baadaye usingizi wa mapenzi ya joto la
Dar es Salaam. Au mnakwenda tu ufukwe wa bahari kufurahia mandhari. Hayo ndiyo
mapenzi ya kweli. Si mapenzi ya kutegemea mfuko kwanza. Fedha na baa
hufuata baadaye. Kinachotangulia mapenzi asilia.
Kwa kina dada mambo pia hayakuwa rahisi. Kijana wa
kikwetu akishakutoa dada, -akikununulia zito, jepesi na la wastani-
ukishafurahi unakuwa sasa mtwana wake. Kuna siku utapigwa. Utasutwa. Iko
miezi utawekwa hata mimba na jamaa hatoonekana kumtunza mtoto. Baadaye
utagundua ala kumbe! Kapata mwingine.
Uafadhali
ulionekana kwa Wamarekani weusi. Warefu, wazungu weusi, wenye tabia tofauti na
zetu. Waliongea kile Kiingereza cha “bradha- man” na “sista-du” kiliichoonekana
kitamu. Wakimbizi na watembezi wa Kimarekani walijazana Tanzania ya kipindi
hicho. Walizikimbia tafrani za Marekani: ubaguzi wa ngozi, harakati za chama
cha Black Panther kilichochukua bunduki kupigana na nguruwe weupe. Hadi leo
haujaisha. Enzi hizo mwanamke wa Kitanzania akimwona “Mniga” (kama tulivyowaita
mitaani) ni kama kumshuhudia mdogo wake Mungu. Astakafurlah! Macho huwatoka kina
dada; ndimi nje. Walijua kuongea na mwanamke, walifuzu mapenzi. Ni kama
Wanigeria wanavyohusudiwa na wanawake wetu leo. Kipya kinyemi. Baadaye
iligundulika hawakuwa tofauti na wanaume wazalendo.
Miaka imevuta miguu; leo wanawake weusi hawataki wanaume weusi
ki- jumla. Mwanaume mweusi hakosi nyumba ndogo au tatu. Mwanamke mweusi
keshamfahamu kaka yake. Keshamjua. Akishamkubalia huba au mahaba, hatokuwa yeye
tu. Hilo limeenea Majuu yote. Limeenea kiasi ambacho dada weusi hawana imani na
kaka zao. Wameanza kusaka Wazungu. Zamani Mzungu hakupendwa sana na mwanamke
mweusi. Wapo dada wachache waliokwenda na Wazungu ndiyo; ila wengi walidai ah
Mzungu hana nguvu kitandani. Au walilalamika wajihi wa ngozi haukuwavutia.
NGOZI IKOJE
SIJUI...
Leo mengine. Kinachotafutwa ni mapenzi na mahusiano si
kitanda au fedha tu..
Hivyo basi,
mapenzi yanayodumu, yanayowezekana ni baina ya mwanamke mweusi na Mzungu.
Sikiliza...
Wakati harakati za
ukombozi wa wanawake wa Kizungu zilizofoka moshi miaka ya Sitini, wanawake
waligeuza mahusiano. Miaka ya Sabini uzunguni kote ulikuwa wakati wa wanawake
kudai usawa makazini, kuwataka wanaume waache udhalimu nk. Leo wanawake wa
Kizungu ndiyo watawala wa nyumba, hata sehemu za kazi za kijamii.
Wanawake wa Kizungu wanatawala mazingira kiasi ambacho kura za kisiasa
zinawaegemea. Hapa Uingereza kuna mfano mzuri, kisiasa.
Mwezi
uliopita Bwana David Cameroon, Waziri Mkuu (na kiongozi wa chama cha
Conservative) alibatilisha baraza lake la Mawaziri. Badala yake alichagua
wanawake zaidi. Inadaiwa kafanya hivyo kutafuta kura za wanawake uchaguzi ujao
wa 2015.
Mbinu hizi zilitekelezwa pia na Waziri Mkuu wa zamani,
Chama cha Leba, Tony Blair, alipoingia madarakani, 1997. Alifanya historia kwa
kuwa na wabunge 101 wa kike , baadhi walishika vyeo vya uwaziri! Waliitwa
“Blair’s Babes.”Hadi leo wengi bado wamo serikalini. Huo ni mfano mdogo
unaodhihirisha namna mahuasino yalivyobadilika kuanzia mapambano ya haki za
akina mama yalipochachamaa Ulaya miaka hamsini iliyokwenda.
Wanawake wanatawala na ni wakali. Baadhi ya wanaume wa
Kizungu huona afadhali kuwa na wanawake wa mataifa mengine – Asia na
Afrika. Hawa nao huwa wamechoshwa na wanaume wasioaminika. Hapa basi watu
wawili hawa walioshakereka, hukutana. Ndiyo maana leo mahusiano baina ya
wanawake weusi na wanaume wa Kizungu yanastawi sana.
Tanzania je? Wengi
wanaandika kuulizia mahusiano na Wazungu.
Ugumu wa maisha unajenga ari za kumpata mgeni
kujiendeleza. Je kuna wepesi na uzito gani?
|