
Baraza la usalama la kitaifa nchini Burundi limesema watu hao waache
uasi wao unaoyatatiza maisha ya watu wa Burundi. Waandamanaji wamepewa
muda wa saa 48 kiviondoa vizuizi vyote walivyoviweka barabarani.
Baraza hilo la usalama linaloongozwa na Rais Nkurunziza limetaka njia
zote zilizowekewa vizuizi na wapinzani hapo awali zifunguliwe na majeshi
ya usalama, katika muda wa saa 48.
Lakini kiongozi wa upinzani Pacifique Nininahazwe ameishutumu amri hiyo
iliyotolewa na serikali na ameiita kuwa ni tangazo la vita. Bwana
Nininahazwe amesema maandamano yataendelea hadi hapo Rais Nkurunziza
atakapouacha mpango wake wa kuwania muhula wa tatu wa urais unaoenda
kinyume na katiba ya nchi.