
KWA wanaofuatilia mpira wa miguu
kwa ukaribu zaidi wanafahamu stori kubwa ya mgomo wa chama cha wachezaji
Hispania (Players Union), wakipinga muswada uliopelekwa Serikalini na
bodi ya ligi, LFP ( ( Liga Nacional de FĂștbol Profesional), chombo
kinachoendesha soka la Hispania.
Muundo wa soka la Hispania kama
wa Bongo vile, Ligi kuu (La Liga) na ligi daraja la kwanza (Segunda
division) zipo chini ya Bodi ya Ligi.
LFP na serikali wameleta muswada
katika makubaliano ya haki za matangazo ya televisheni wakitaka
makubaliano yafanyike kwa pamoja kama ligi kuu England, lengo lao ni
kuongeza ufanisi kwa kuzinufaisha timu zote kuliko ilivyo sasa ambapo
klabu zinakubaliana zenyewe na makampuni yanayorusha moja kwa moja
‘Laivu’ mechi za ligi kuu na ligi daraja la kwanza.
Kinachotokea Hispania ni kwamba,
FC Barcelona na Real Madrid wana ushawishi na mvuto mkubwa,
wanafuatiliwa sana, hivyo makampuni mengi hivi sasa yanavutiwa kuingia
mikataba na klabu hizo mbili, matokeo yake nusu ya pesa inayolipwa kwa
ajili ya haki za matangazo ya televisheni inachukuliwa na miamba hii ya
soka nchini humo.
Madhara yake ni kwamba klabu hizi
mbili zimekuwa na msuli mkubwa wa fedha kuliko klabu nyingine na ili
kuweza kupunguza pengo lililopo, serikali ambayo inanufaika pia na haki
za matangazo ya Telesheni kwasababu wachezaji wanalipa kodi imeona ni
bora kubadilisha mfumo.
Mishahara inapoongezeka kwa
wachezaji, kodi nayo inaongezeka, ili kuongeza pato, serikali inaona ni
bora kuwepo na makubaliano ya pamoja katika haki za matangazo ya
Televishei wakiamini wanaweza kuzisaidia klabu nyingine za chini ili
ziweze kupata ‘mzigo’ wa maana na kuweza kulipa mishahara ya maana kwa
wachezaji ambao wanalipa kodi serikalini.
Lakini kilichosababisha mgomo
unaoendelea hivi sasa ni kutoshirikishwa kwa chama cha soka Hispania
kwenye huo mpango unaosimamiwa na serikali ya Hispania na chombo huru
kinachoendesha ligi yaani Bodi ya Ligi (LFP).
Chama kimeamua kusimamisha
michezo yote mpaka pale watakapokaa meza moja na serikali pamoja na FLP
kwa lengo la kutetea maslahi yao kwasababu katika mgao mpya uliokuja
unaonesha chama cha soka kina mgao wa asilimia 4 ya jumla ya fedha zote
zinazotokana na haki za matangazo ya televisheni na wameona ni kidogo.
Zaidi chama kinaona kimepunjwa
kwenye ule mchakato wa awali na wanaamini kama wangeshirikishwa
wangekuwa na hoja za msingi za kuwafanya waweze kupata mzigo wa maana.
Lakini upande wa pili, chama cha
wachezaji (Players Union) kimeungana na chama cha soka kupinga muswada
huo wakisema kuna baadhi ya vipengele vitakavyoendelea kuwanyonya
wachezaji.
Wanapointi mbili, mosi; pamoja na
gawio ambalo baadaye watakuja kupata pamoja kwa maana ya klabu za ligi
kuu na daraja la kwanza, bado timu za Segunda division zitapata kiasi
kidogo cha fedha ambazo haziwezi kusaidia.
Pili; wale wachezaji wa Ligi kuu
(La Liga) wakiangalia vipengele vya pamoja kwenye mgawanyo mpya wa haki
za Matangazo, hawaoni nafasi ya klabu za chini kupata hela ya maana na
matokeo yake wachezaji wa chini hawatanufaika na mfumo huu mpya.
Pia wachezaji hao wanaocheza ligi
kuu wanasema ule mgawanyo mpya utawaathiri wao kwasababu hauongezi pato
kwa klabu zao zaidi ya kutengeneza mazingira ya pesa nyingi kwenda
serikalini.
Wanaamini kama watakubali mfumo
huo itafika mahali klabu zitapunguza mishahara yao kwasababu pato
litapungua ikiwa ni matokeo ya utaratibu mpya ambao watu wengi wanaamini
ndio suluhusisho la uchumi wa soka la Hispania katika ngazi ya klabu.
Kutokana na sababu hizo wameamua kugoma kwenda kujadili muswada huo
mpaka pale ambapo baadhi ya vipengele vitakapoangaliwa upya.
Kutokana na suala hili kuna jambo
muhimu la kujifunza ukija katika mchakato wa huku kwetu Tanzania.
Mkataba wa haki za Matangazo ya Televisheni walioingia Azam TV na bodi
ya ligi kuu (TPLB) unakufanya ujifunze kirahisi kuwa kuna rushwa
ilitembea, huhitaji kwenda shule ili kufanya uchunguzi kugundau kuwa
rushwa ilitembea wakati wa mchakato wa kusainiwa kwa mkataba ule.
Katika hali ya kawaida,
haiwezekani kwamba klabu zote zipate gawio sawa kutokana na haki za
matangazo ya televisheni (Milioni 100 kutoka Azam TV).
Huu mgogoro unaondelea Hispania
baina ya chama cha soka, chama cha wachezaji, bodi ya ligi na serikali
unatufumbua macho sisi tuliopo dunia ya mbali ili walau tuweze
kujifunza. Ingawa si kwa kufuata kila kitu kwasababu wenzetu wameendelea
sana, lakini ni muhimu kupata maarifa machache ambayo tunaweza
kuyatumia katika mazingira ya kwetu kwa lengo la kupata tija katika soka
letu.
Cha kwanza, kwa muundo wa bodi ya
ligi kuu ya kwetu inayohusisha ligi kuu na ligi daraja la kwanza, timu
zote za ligi kuu na ligi daraja la kwanza zinatakiwa kunufaika na haki
za matangazo ya Televisheni kwasababu mkataba unasainiwa kati ya bodi
ya ligi na Televisheni (Azam TV) ambayo inaundwa na timu za ligi kuu na
ligi daraja la kwanza.
Haiwezekani kila mapato
yanayopatikana katika bodi yasizihusu klabu za ligi daraja la kwanza,
yaani sawasawa na wewe una watoto wa kuwazaa nyumbani kwako na watoto wa
mjomba au Shangazi, unapika chakula, lakini ikifika wakati wa kupakua
msosi unawaambia watoto wa Shangazi au mjomba kwamba ‘chakula hiki
hakiwahusu’.
Watoto wote wanaishi kwenye
familia moja (timu za ligi kuu na daraja la kwanza), ingawa watoto wako
wa kuwazaa wanaweza kunufaika zaidi, lakini lazima watoto wengine
wanufaike pia kwa kiasi fulani.
Kitu walichotufumbua macho
Hispania ni kwamba; mikataba yote wanayoingia Bodi ya ligi kuu, klabu za
ligi daraja la kwanza zihusishwe wakati wanakwenda kufanya mazungumzo
ya haki za matangazo ya Televisheni kwasababu nao ni sehemu ya wanachama
wa bodi.
Lazima zihusishwe kwa maana ya
maamuzi ya pamoja katika haki za matangazo. Kwa mfano Azam TV kwa
kutotambua wanaweza kutumia fedha nyingi kuingia mkataba wa ligi kuu na
ligi daraja la kwanza, kumbe wao wana haki ya kukubaliana kwa pamoja
kwasababu wanafikia makubaliano na bodi ya ligi na sio klabu moja moja.
Kama wangekuwa wanakubaliana na timu moja moja, wangeweza kuchagua
Simba, Yanga na Azam.
Kwa vile wanakubaliana na bodi
ambayo inajumuisha klabu za ligi kuu na ligi daraja la kwanza, Azam TV
wao wanatakiwa kuja na fedha ya pamoja, halafu bodi wao ndio wanakaa
chini kutengeneza gawio la pesa kwa klabu za ligi kuu na daraja la
kwanza.
Kwasababu klabu za ligi kuu mechi
zao zinaoneshwa nyingi wanaweza kupata asilimia 90 na klabu za ligi
daraja la kwanza zipate asilimia 10 kwa kuwa mechi zao zinaoneshwa
chache.
Kingine cha kujifunza ni nguvu ya
wachezaji katika mikataba, kwa mfano chama cha wachezaji cha soka la
Hispania kinagoma kucheza kwasababu wanaona vipengele vilivyomo katika
mkataba vikisainiwa bila chombo chao kuhusishwa kitawaathiri wao moja
kwa moja katika mazingira makuu mawili,
Kwanza ule mkataba ukisainiwa, mapato yao kwa maana ya mishahara na bonasi vitapungua kutokana na klabu kushuka kimapato.
Pili; mfumo huu haujengi
mazingira mazuri kwa hawa ambao tunasema hawana kitu (timu za segunda
division). Utaratibu mpya hauji kuwafanya wapate zaidi bali unakuja
kuwadidimiza. kwahiyo wao kama chama cha wachezaji wameungana na chama
cha soka kugoma kwasababu kwenye huo mkataba hakuna mazingira ya wao
kama wahusika wakuu kunufaika.
Ukija kwetu Bongo ukilinganisha
na haya yanayofanyika Hispania, kumbe hata hii mikataba wanayoingia bodi
ya ligi, wachezaji nao wanatakiwa kuwa na chama chao kinachoweza
kuungana kugomea vipengele vya mikataba vinavyowanyonya wao.
Chama cha wachezaji kinatakiwa
kuwa na wanasheria, wataalamu ambao wanaingia kwenye vikao na
kuwasilisha maslahi ya wachezaji. Haimaanishi Jonas Mkude kuwa mchezaji
wa Simba, basi Simba wana mamlaka yote ya kufanya chochote, lazima
kuwepo mipaka, uhusiano wa klabu na mchezaji upo uwanjani kwa kufunga
magoli na kucheza dakika 90, lakini linapokuja suala la maslahi pamoja
na biashara linaangalia kwa jicho lingine, wachezaji wanatakiwa kuwa na
watu wanaowasimamia.
Mchezaji lazima naye apate
stahiki yake katika mikataba inayosainiwa, ukiangalia wachezaji wa ulaya
kama Cristiano Ronaldo, klabu yake ya Real Madrid ina mkataba na
kampuni ya Adidas kwa ajili ya kuwavalisha jezi wachezaji, kwasababu
Ronaldo anachezea timu ambayo ina mkataba na Adidas basi analazimika
kuvaa jezi ya Adidas, lakini mchezaji halazimishwi kuvaa kiatu cha
Adidas kwasababu mguu ni wake mwenyewe.
Ndio maana Ronaldo anavaa kiatu
cha Nike kwasababu ana mkataba nao binafsi kama mchezaji. Akiwa katika
mazingira ya nje ya klabu anavaa nguo za Nike, akiwa anafanya mkutano na
waandishi wa habari unaomuhusu yeye na mambo yake anavaa nguo ya Nike,
lakini akiwa anafanya kwa kuiwakilisha klabu, anavaa nguo za klabu
ambazo ni Adidas.
Hii maana yake ni kwamba,
wachezaji wana nguvu, wana nafasi kubwa kwa kila kinachofanywa na klabu
au chombo chochote kinachosimamia mpira na kuingiza pato kwa
kumuhusisha yeye.
Ndio maana wacheza nchini
Hispania wanaamua kugoma kwasababu ule mkataba unawaathiri moja kwa moja
na wanaona wakiingia mkataba huo mpya mapato yao yatashuka kwasababu
klabu badala ya kupata kwa mfano milioni 100 sasa itapata milioni 70.
Kama klabu itashusha kimapato,
maana yake itarudi huku chini kukata baadhi ya gharama za uendeshaji
ikiwemo kupunguza mishahara kutokana na chanzo mojawapo cha mapato
kupungua (haki za matangazo ya Televisheni).
Wachezaji wa Kibongo wajitambue
kwa kuangalia wachezaji wa Hispania walivyoanzisha mgomo wakitetea
maslahi yao bila kujali kama muswada ule una faida au hapana. Wao
wanatumia wataalamu wao ambao wapo kwenye chama chao, wanatetea maslahi
yao, wanawaeleza kuwa humu ndani ya mkataba kuna vipengele ambavyo
keshokutwa vitawaathiri ninyi moja kwa moja, wao kama wawakilishi wa
chama hawakubaliani na vipengele hivyo na wamewataka wachezaji kutumia
nguvu yao kugoma.
Kibongobongo, tunapoelekea
kusaini mikataba mipya, lazima tukubali kutumia wataalamu wenye uelewa
wa kujadiliana kuhusu haki za matangazo ya Televisheni ili watetee
maslahi ya klabu pamoja na wachezaji.
Klabu ziwe na chombo chao chenye
watu wenye uelewe, ambao wanakwenda kutetea maslahi ya klabu. Pia wawepo
viongozi wa klabu wanaotetea maslahi ya wachezaji.
Kilichopo Bongo, ‘Third Part” kwa
maana ya makampuni wanapata urahisi kwasababu viongozi wengi wa mpira
hawaendi kutetea maslahi ya klabu wala wachezaji, wapo kwa ajili ya
kutetea maslahi yao na ndio maana unakuta madhamini anakuja anasaini
mkataba rahisi kwasababu wanaokwenda kufanya mazungumzo ya mkataba
hawana taaluma yoyote, wanarubuniwa kirahisi kwa kupewa hela (rushwa)
ili waweze kukubali matakwa ya makampuni ya udhamini na kuridhia
kusaini mikataba ambayo wadau na wataalamu wa soka wanaona ni ‘Bomu’.
Nawatakia siku njema!
Source: Shaffihdauda.co.tz